Thursday, March 8, 2012

WENGER AFURAHIA ARSENAL KUFA KIUME


 
 KOCHA Arsene Wenger amewaambia wachezaji wake Arsenal kwamba wana kila sababu ya kujipongeza kutokana na ushindi wa mabao 3-0 walioupata dhidi ya AC Milan, ingawa haujawasaidia kusonga mbele hatua inayofuata ya Ligi ya Mabingwa soka Ulaya.
Ikiwa nyuma kwa mabao 4-0 katika mechi ya kwanza kwenye Uwanja wa San Siro, Arsenal ilikosa nafasi ya kucheza hatua ya 8-bora, lakini ilionyesha kiwango kizuri kwenye mechi hiyo ya marudiano.
Mabao ya Laurent Koscielny, Tomas Rosicky na lile la penalti lililofungwa na nahodha Robin van Persie, yalitosha kumfurahisha Kocha Wenger kwenye Uwanja wa Emirates.Nahodha Van Persie angeweza kufanya matokeo kuwa ya ajabu kama angetumia vizuri nafasi nzuri kufunga ambayo ingeipa timu yake bao la nne.
"Ni lazima wafurahie kiwango kizuri walichoonyesha," alisema Wenger wakati akiongea na Sky Sports 2.
"Timu ilionyesha mchezo mzuri na umoja katika kupambana baada ya mechi ya kwanza, lakini hayakuweza kutuvusha. Tulikuwa na nafasi kadhaa za kufunga, lakini siyo mbaya kwa sababu tumeweza kuendeleza mfululizo wa ushindi jambo ambalo ni muhimu kwetu.
"Tumelipa kwa matokeo mabaya ya mchezo wa kwanza. Lakini tumejipa kila kitu, hili ndilo unaloweza kulifanya kwa kiwango cha juu zaidi na kukubali kupokea matokeo."
Katika mechi hiyo, Arsenal iliwakosa majeruhi pacha Aaron Ramsey na Mikel Arteta katika nafasi ya kiungo, lakini ilifurahishwa na uchezaji wa Alex Oxlade-Chamberlain. Wenger anaamini kama viungo hao wangecheza basi kikosi chake kingeweza kupata matokeo tofauti.
"Kulikuwa na mapungufu sehemu ya kiungo na hii ilipelekea kuchoka kipindi cha pili, tulihitaji kuumiliki zaidi mpira kipindi hicho. "Naamini tulikuwa na uwezo wa kutosha na tungeweza hata kufunga mabao mawili zaidi."
Van Persie amekuwa shujaa wa mabao kwa Arsenal msimu huu, angeweza kufunga bao la nne kama si jitihada za kipa Christian Abbiati kuokoa shuti lake.
Alipoulizwa kuhusu nafasi hiyo waliyopoteza mshambuliaji wake, Wenger said: "Nadhani alitaka kumchota kipa, kwa sababu Abbiati alikuwa chini na alinyanyuka haraka na kuucheza mpira, hatukuweza kufunga."
Kocha wa Milan, Massimiliano Allegri alinusurika kushuhudia timu yake ikinyanyaswa kwenye Uwanja wa Emirates.
"Tulicheza vizuri tukiwa na washambuliaji wawili mbele, lakini haikutusaidia.
"Tulifungwa katika kona ya kwanza na hii ikaleta tofauti kubwa kiasikolojia, na baada ya hapo tulifanya makosa mengi hasa sehemu ya kiungo. "Naweza kusema kwamba, tulicheza vibaya kabisa, tulikuwa chini ya kiwango zaidi ya kujilinda. Kipindi cha pili tulicheza kwa kushambulia.
"Ni kipigo cha aibu, lakini muhimu kwetu ni kucheza hatua nyingine. Sasa tuna wakati wa kuwa na wachezaji kadhaa uwanjani ambao walishindwa kuwapo kutokana na kuwa majeruhi. Sikuiona timu katika hali ya wasiwasi kuna wachezaji wenye uzoefu mkubwa hapa," alisema.
Benfica ilionyesha mchezo wa kuvutia na kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Zenit St Petersburg na kupata nafasi ya kucheza hatua ya nane bora Ligi ya Mabingwa soka Ulaya.Katika mchezo wa kwanza, Benfica ililala kwa mabao 3-2 katika mechi ya ugenini ambako kulikuwa na baridi kali kwenye Uwanja wa Stadion Petrovskiy.

No comments:

Post a Comment