Sunday, April 29, 2012

BARAZA JIPYA LA MAWAZIRI TANZANIA..........

Rais Kikwete akiwa na mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali Bwana Ludovick Utouh.

Taarifa ya Rais Kikwete kutaka kuvunja na kuunda upya Baraza la Mawaziri ilitangazwa juzi na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM, Nape Nnauye alipokutana na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kumalizikia kwa kikao cha dharura cha Kamati Kuu ya CCM.
Hatua hii imekuja baada ya udhaifu mkubwa wa kiutendaji kujidhihirisha  katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Bw. Ludovick Utouh. Mawaziri katika wizara mbalimbali wameshindwa kuwajibika ipasavyo kwa umma na hivyo kuisababishia nchi hasara kubwa.
Kuundwa kwa baraza la mawaziri kunatoa imani kubwa kwa Watanzania walio wengi ambao wamekuwa watumwa wa fikra juu ya walafi wachache waliogeuza wizara zetu kama sehemu ya kujinufaisha kiuchumi kupitia fedha za walala hoi.
 Baraza jipya la mawaziri linatabiriwa kuundwa na idadi kubwa ya Vijana wachapakazi, wazalendo wa nchi na wawajibikaji. Miongoni mwa Vijana wanaotajwa kuwa huenda wakaingia katika Baraza jipya la Mawaziri ni pamoja na Mbunge wa Bumbuli, Januari Makamba, Mbunge wa Busega, Dk Titus Kamani, Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi, Mbunge wa Handeni, Dk Abdallah Kigoda, Mbunge Kahama, James Lembeli, Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola, Mbunge wa Same Mashariki, Anna Kilango na Mbunge wa Igunga Dk Dalaly Peter Kafumu.
Mwingine anayetajwa kuingia katika baraza hilo ni aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk. Asha Rozi Migiro ambaye anatarajiwa kurejea nchini hivi karibuni baada ya kumaliza mkataba wake wa kuutumikia umoja huo.

Imani ya kuundwa kwa baraza jipya la mawaziri haitunyimi nafasi ya kuwaza juu ya mfumo wa uongozi katika nchi yetu. Kuifikiria zaidi mianya ya Rushwa na Uwezekano wa ubadhirifu katika sekta mbalimbali za Umma ni suala la msingi.



No comments:

Post a Comment