Tuesday, April 17, 2012

MWENYEKITI WA UMOJA WA VIJANA CCM( UVCCM ) AHAMIA CHADEMA


Aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi ( UVCCM ), Mkoa wa Arusha Bwana James Millya amekihama Chama hicho na kujiunga na Chama cha Democrasia na Maendeleo ( CHADEMA )
Bwana Millya alitoa tamko la kukihama Chama cha Mapinduzi (CCM ) katika mkutano na waandishi wa habari mkoani arusha.Millya amesema aliamua kukihama CCM na kuhamia CHADEMA ili aungane na wanaharakati wenzake katika kutetea maslahi ya walio wengi.

“Natangaza rasmi kujitoa CCM na kujiunga na Chadema ili kuendeleza harakati za kulikomboa taifa hili kutoka mikononi mwa watu wachache wenye fikra kwamba wao ndio wenye hatimiliki ya nchi hii,” alisema Ole Millya
Alisema amegundua kuwa alikuwa akichezea timu isiyo na uwezo wala nia ya ushindi katika ulingo wa siasa na uongozi wa umma na kujipa moyo kwamba licha ya kuchelewa kugundua kosa hilo, sasa amegundua na anakihama Chama hicho.

Ole Millya aliahidi kuwa kundi kubwa la vijana wa CCM wako nyuma yake na wanasubiri muda muafaka kuhamia Chadema.

Mwaka jana, Ole Millya aliingia kwenye mgogoro mkubwa na viongozi wa CCM Mkoa wa Arusha hadi kupewa karipio kali kwa tuhuma za kumtolea maneno machafu Katibu wa chama hicho Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda.
Kabla ya Uchaguzi Mkuu uliopita, Ole Millya anayeaminika kuwa mfuasi mtiifu wa Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa aliingia kwenye mgogoro mkubwa na Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka alipodai kupigwa na kutishiwa kwa bastola.

Alimshtaki Ole Sendeka mahakamani ambaye aliachiwa huru baadaye baada ya kukosekana kwa ushahidi.

Baada ya Millya kutangaza kung'atuka CCM mkoani Arusha, viongozi wa chama hicho, akiwamo Katibu Mkuu, Wilson Mukama, Katibu wa Uenezi na Itikadi, Nape Nnauye, Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigella, Makamu Mwenyekiti wa UVCCM, Benno Malisa, Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Loota Sanare, walitoa matamko mbalimbali.

Viongozi wa CCM walieleza kuwa hatua yake hiyo, hakuna madhara yeyote kwa CCM.
Mukama alisema Millya alikuwa chini ya karipio kali na alikuwa amebakiza hatua moja kufukuzwa kwa sababu ya usumbufu na mtovu wa nidhamu.
Nnauye alituma ujumbe kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook uliosomeka: “Nampongeza Millya kwa kuamua kukisaidia chama changu, kwani alishakuwa mzigo mkubwa kwa CCM. Itakumbukwa alikuwa afukuzwe kwenye chama kutokana na mambo alokuwa akifanya. Akapewa karipio ili apate muda wa kurekebisha tabia yake! Kaondoka akiwa chini ya karipio. Kajivua gamba, tunampongeza kwa kuitikia wito wa kujivua gamba. Kila la kheri aendako ni kijana bado anayo mengi ya kujifunza.

Kwa upande wake, Chadema kimefurahia hatua hiyo ambapo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe aliwaambia waandishi wa habari mjini Dodoma kwamba Chama chake kinampokea Millya kwa mikono miwili na kinaamini kuwa atakuwa na mchango mkubwa.

No comments:

Post a Comment